Friday, 19 July 2013

PAUL MFEDE 'BOLINGO' - SIMBA ASIYESHINDIKA ALIYESHINDWA NA KIFO - SHUJAA WA CAMEROON MWAKA 1990 KWENYE KOMBE LA DUNIA ALIYEPOTEZA MAISHA BAADA YA KUSHINDWA KULIPIA MATIBABU



Louis Paul Mfede alikuwa gwiji wa soka nchini Cameroon , alikuwa shujaa ndani ya uwanja na balozi mzuri nje ya uwanja .

Fefe aka Bolingo alikuwa sehemu muhimu ya kikosi kilichoipeleka Cameroon kwenye robo fainali ya kombe la dunia mwaka 1990 na kuweka historia ambayo haijafikiwa mpaka hii leo .

Lakini tarehe 10 mwezi uliopita alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 52 kutokana na maradhi ya mapafu kwenye hospitali moja huko Yaounde na sababu za kifo chake zaidi ya maradhi ilikuwa ukweli kuwa alishindwa kugharamikia dawa na matibabu ya maradhi yake . 


Jeneza la Mfede wakati akienda kuzikwa

Ulikuwa ni mwisho wa kuhuzunisha kwa maisha ya mtu ambaye aliifanyia Cameroon makubwa sambamba na watu kama Roger Milla , Thomas Nkono, Libih Thomas, Maboang Kessack na wengineo hasa miaka 23 iliyopita nchini Italia kwenye kombe la dunia.

Mafanikio ya Mfede na wenzie yaliwafanya Wacameroon wote kujawa na matumaini na kumbukumbu ya wengi waliomshuhudia akiwapiga chenga wachezaji watatu pamoja na tabia yake ya kuwafanya wenzie wajiamini hadi kuwafunga Argentina 1-0 kwenye mchezo wa kwanza wa kombe la dunia mwaka 90 haitafutika vichwani mwa watu wa Cameroon.

Pamoja na yote haya, viongozi wa chama cha soka cha Cameroon na wizara ya michezo waliotaarifiwa na mkewe Paul juu ya hali ya mumewe hawakufanya chochote .

Mtoto wa Mfede anayeitwa Frederick alifichua kuwa msaada pekee ulitoka kwa Roger Milla ambaye alisaidia kulipa gharama za hospitali wakati familia yake ikiwa imekosa msaada. Siku ya mazishi yake, waziri wa michezo Adam Garoua alimtunuku Mfede medali ya heshima kwa mchango wake kwa taifa la Cameroon huku akiweka shada la maua kwenye kaburi lake kwenye kijiji cha Nkol-kosse huko Lekie kwenye jimbo la kati la Cameroon lakini watu wamehoji kwanini Mfede hakupewa huduma wakati akiwa mgonjwa huduma ambayo ni muhimu kuliko hata nishani isiyo na maana wakati huu akiwa amekufa.


Kikosi cha Cameroon kilichofanya maajabu 1990 - Mfede aliyechuchuma wa kwanza mkono wa kulia.

Thomas Nkono alilalamika, "Kwanini watu ambao tuliwahi kuitwa mabalozi leo hii maisha yetu yanafifia kwa aibu na shida . Ninapoona watu wachache ambao ni mashabiki halisi wa soka wakiwa wamelizunguka jeneza la Mfede nasikititka huku nikisema kuwa hii ni mbaya kwa shujaa wa taifa . Inauma kuona akiondoka duniani kama mtu ambaye hakuna anayemfahamu."

Thomas Nkono ambaye anaaminika kuwa kipa bora wa afrika kwa miaka yote aliongeza kuwa, "Watu ambao walijitoa kwa ajili ya soka wanapaswa kutambuliwa na serikali lakini kumuona Mfede anakufa mtaani namna hii inaniuma sana."

Beki wa zamani Benjamin Massing alisema, "Ni huruma sana kumuona mwenzetu amekufa kwa namna kama hii akiwa ametelekezwa na kauchwa mwenyewe."







Mfede akimtuliza Rigobert Song baada ya kupewa kadi nyekundu kwenye moja ya mchezo wa kombe la dunia 1990

 

Pamoja na kukosekana kwa huduma na mazishi ya kitaifa kwa Mfede au the magic foot yaani guu la kushoto la kichawi kama alivyokuwa akifahamika enzi za miaka ya themanini jina ambalo alipewa na mchezaji bora wa afrika mwaka 1980 Jean Manga Onguene atakumbukwa na wenzie kama mtu mwenye furaha na aliwaunganisha wachezaji wenzie .

"Kesi ya Mfede ni kesi ambayo inawakuta wachezaji wengi wa zamani wa Cameroon hasa wale wa miaka ya tisini .

Sisi wanasoka hakuna anayetujali
," anasema mchezaji wa zamani Libih , anaongeza, "Mbaya zaidi hakuna umoja miongoni mwetu kwa kuwa sio serikali pekee ambayo itafanya kila kitu . Ni kweli kuwa tunajitolea maisha yetu kupigania bendera ya taifa letu lakini baadaye tunakuwa watu wa kawaida lazima tukutane na maisha ya baada ya soka. 

Inatia huruma kuwa wachezaji wakubwa hawaweki misingi yoyote ya kulinda maslahi yetu . Tunakimbilia maisha mabaya ambayo hayafahamiki na ndio maana tunapambana kwenye televisheni kwa kuwa tunataka kurudi mahala fulani, inatia huruma na maisha ni magumu, tunapigana sisi kwa sisi badala ya kujenga."

Mchezaji mwingine Youmbi Ayakan ambaye alicheza kwenye miaka ya tisini aliungana na Libih ambapo alisema kuwa kuna haja ya wachezaji kujipanga na kuweka hali zao za baadaye kuwa nzuri zaidi. "Ni muhimu kwa wale wanaocheza sasa na hata wale waliostaafu, wachezaji wengi wa sasa hata hawafahamu kaka zao waliocheza kabla yao, sisi ndio tuliwafanya waote kufikia mahali hapa walipo leo hii lakini hakuna anayefanya kitu kwa ajili yetu."

Suluhisho la tatizo hili kwa mujibu wa Libih ni kwa wachezaji waliostaafu kutumia uwezo wao kuwasaidia wachezaji wachanga ama kuwa viongozi wa chama cha soka na tawala nyingine za michezo na hata kuingia kwenye ukocha

"Kuna haja ya chama cha soka kulinda maslahi ya wachezaji kwa kuwa sisi wote tumefanya makubwa kwa niaba ya taifa na kuna haja ya wanamichezo wote kwa pamoja kulindwa."

SAKATA LA USAJILI WA ROONEY : FAMILIA YAANZA KUATHIRIKA - MKEWE HATAKI WAHAMIE NJE YA NCHI

Sakata la usajili la mshambuliaji WAYNE Rooney jana usiku lilitishia kuivunja familia yake — kwa sababu mkewe wake Coleen hataki kuhamia nje ya nchi hiyo.

Man United jana ilikataa ofa inayotajwa kuwa £20million kutoka Chelsea, mahala ambapo mshambuliaji huyo inasemekana yupo radhi kwenda kwa kuwa Coleen, 27, ataendelea kuwa karibu na wazazi wanaoishi huko Liverpool.
Coleen Rooney with eldest son Kai
Lakini United wanaonekana hawapo tayari kuwauzia silaha wapinzani wao wa moja kwa moja ndani ya ligi kuu ya England - hivyo kufanya kuwepo na uwezekano mkubwa wa uhamisho wa kwenda Paris Saint-Germain kufanikiwa kama Moyes akiamua kumuuza Rooney.
Wayne Rooney at training ground 
Chanzo kimoja cha habari kilisema: “Suala hili la uhamisho wa Rooney linasababisha hali tete baina ya Wayne na Coleen. Hawataki kuhamia nje ya nchi. Lakini ikiwa hatashindwa kuhamia Chelsea basi mambo yatazidi kuwa magumu kwao. 
“Chaguo la kwanza la Wayne ni Chelsea kwa sababu wakihamia kusini mwa nchi bado wataendelea kuwa karibu na Liverpool wakiendesha masaa kadhaa kwenda mahala wazazi wao wanapoishi.
“Lakini United wamesema kwamba, ikiwa watamuuza - itakuwa ni kwa klabu ya nje tu, hivyo PSG wanaweza wakarudi na ofa nzuri. 
"Coleen hataki kabisa kwenda Ufaransa kwa sababu anadhani ni mbali sana na ilipo familia yake, ambao wanamsaidia sana katika kulea wanae Kai na Klay.
"Hivyo ikiwa atauzwa, Wayne itabidi atumie ndege binafsi kutoka Paris-Liverpool, au aende kuishi mwenyewe hotelini.”

Mchana wa jana mke wa Rooney, Coleen alijikuta tena kwenye majibizano makali na baadhi ya mashabiki kwenye mtandao wa Twitter ambao walikuwa wakimtumia meseji ampelekee Rooney kuhusu suala la uhamisho wake - hali ambayo inazidi kuleta hali tete.

WAKATI KOCHA WAO AKIUGULIWA NA MAMA YAKE - MAN CITY WAZIDI KUIMARISHA TIMU YAO - NEGREDO NA JOVETIC WASAJILIWA


MANUEL PELLEGRINI amesafiri kwenda kwao Chile jana usiku wakati Manchester City ikikamilisha usajili wa £39million wa washambuliaji wa wawili.

Kocha huyo aliiacha klabu yake ikiwa kwenye kambi ya mazoezi nchini South Africa kwa sababu anauguliwa na mama yake mazazi.

City wana matumaini Pellegrini, 59, ataungana na kikosi chake tena huko Hong Kong jumanne ijayo — akiungana na washambuliaji wapya wa timu hiyo Alvaro Negredo na Stevan Jovetic.
Negredo akienda kufanyiwa vipimo vya afya
Bosi msaidizi wa klabu hiyo Brian Kidd alisema: “Manuel imembidi arudi nyumbani kwao Chile. Tuna matumaini ataungana nasi tukiwa Hong Kong jumanne lakini hatuna uhakika." 

Mshambuliaji wa kihispaniola Negredo, 27, jana mchana alikuwa jijini Manchester kwenye hosptiali ya Bridgewater akifanyiwa vipimo kukamilisha uhamisho wake wa kutoka Seville kwa ada ya uhamisho ya kuanzia ya £16.4m — huku £4.2m zitalipwa kutokana na kiwango cha mchezaji.
City pia tayari wameshakubalina ada ya usajili ya £22.4 kwa ajili ya mshambuliaji wa Fiorentina Stevan Jovetic.
Mshambuliaji huyo wa Montenegro, 23, atawasili jijini Manchester leo kukamilisha dili hilo la usajili. 
Jovetic alisema: “Mimi bado kijana na nataka kubadilisha maisha yangu ya kisoka.
“City ni timu kubwa na muhimu ndani ya Premier League.
“Nataka kushinda makombe na pia nitakuwa na rafiki yangu mkubwa Matija Nastasic.”

L.A LAKERS YATAKA KUMUUNGANISHA KOBE NA AIDHA LeBRON JAMES AU CARMELO ANTHONY


Timu ya mpira wa kikapu Los Angeles Lakers wanajiandaa kuimarisha timu yao kwa kutaka kumsajili LeBron James au Carmelo Anthony baada ya msimu ufuatao wa ligi, ESPN inaripoti. 
Mastaa wote wawili LeBron na Anthony watakuwa huru msimu ujao ikiwa wataamua kutoongeza mikataba yao ya sasa na vilabu vyao. Kunfi la wachezaji wengine wa kikapu, akiwemo Dwyane Wade, Amar’e Stoudemire na Chris Bosh wana kipengele cha uhuru wa kukatisha mikataba yao, katika mikataba ya miaka mitano waliyosaini mwaka  mapema 2010.
Luol Deng, Danny Granger, Andrew Bogut na Dirk Nowitzki watakuwa huru mwishoni mwa msimu ujao wa ligi ya NBA. Pia L.A Lakers itabidi kufanya uamuzi kuhusu hatma ya Kobe Bryant, ambaye yupo atakuwa anaingia kwenye mwaka wa mwisho wa mkataba wake msimu huu unaokuja.

LeBron James, ambaye ni mshindi wa tuzo ya NBA Finals MVP, alisema hivi karibuni kwamba hafikirii kabisa kuhusu mkataba wake utakapoisha mnamo mwaka 2014.
Lakers walimpoteza Dwight Howard wakati alipoamua kusaini mkataba wa na Houston Rockets badala ya kuongeza mkataba wa miaka mitano na timu hiyo ya L.A

TOP 100 YA WAFUNGAJI BORA WA LIGI KUU YA ENGLAND - THIERRY HENRY NA HASSELBAINK NDIO WACHEZAJI WA KIGENI PEKEE WALIO NDANI YA TOP 10 -



Wakati zikiwa zimebaki takribani siku 30 kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi kuu ya England - hii ndio listi ya wafungaji bora wa muda wote wa ligi kuu ya England.
Inayoongozwa na Alan Shearer ambaye amefunga jumla ya mabao 260, akifuatiwa na Andy Cole na mfaransa Thierry Henry akishika nafasi ya 3 - huku yeye na mshambuliaji wa zamani wa Chelsea Jimmy Floyd Hasselbaink wakiwa ndio wachezaji pekee kutoka nje ya United Kingdom kuwemo ndani ya Top 10.


JUAN SEBASTIAN VERON ARUDI DIMBANI - AFUATA NYAYO ZA BECKHAM KWA KUTOA MSHAHARA WAKE WOTE KUCHANGIA KITUO CHA KUFUNDISHIA SOKA

Juan Sebastian Veron alimaliza miaka yake 18 ya kucheza soka akiwa na klabu ya Estudiantes mwaka 2012 — hii klabu ambayo alianzia kucheza soka. Veron aliendelea kuitumikia klabu hiyo akiwa kama mkurugenzi wa michezo, huku akicheza soka la mchangani na timu ya ndogo ya Brandsen. Kwa bahati nzuri akiwa na klabu hiyo ndogo walishinda ubingwa wa ligi ya La Plata na inaonekana ubingwa huo umempa hamasa ya kurudi dimbani kiungo wa zamani wa Man United mwenye miaka 38 ambaye sasa ameamua kuichezea klabu ya Estudiantes.
Kutoka Reuters:
Veron, ambaye ni mkurugenzi wa michezo wa klabu ya Estudiantes, amesaini mkataba wa kuwa mchezaji wa mwaka mmoja na atacheza msimu wote wa 2013-14 wa ligi kuu ya Argentina.
"Sidhani kama nipo kwenye fomu niliyokuwa nayo mwaka  (2009) wakati tuliposhinda ubingwa wa Libertadores Cup, lakini sasa nimehamasika zaidi kurudi uwanjani kwa sababu napenda kucheza soka," alisema Veron alippongea na Radio Del Plataearlier wiki hii.
Pia labda kwa kufuata mfano wa mchezaji mwenzie wa zamani wa Man United - David Beckham, Veron ameamua kwamba atachangia mshahara wake wote kwenye kituo cha soka ambacho alijifunzia soka miaka 20 iliyopita.

NDOTO ZA KUREJEA UNITED ZAZIDI KUFUTIKA - CRISTIANO RONALDO AIWEKA SOKONI NYUMBA YAKE YA JIJINI MANCHESTER


Matumaini ya mashabiki wa Manchester United kuona kipenzi chao Cristiano Ronaldo akirejea kuitumikia klabu hiyo jana yalizidi kupotea baada ya mchezaji huyo kuiweka sokoni nyumba yake aliyokuwa akiishi wakati yupo nchini England kabla ya kujiunga na Real Madrid.
Ronaldo, 28 — aambaye alijiunga na Real Madrid kwa ada ya uhamisho wa £80million mnamo mwaka 2009 — amekuwa akiuhusishwa sana kurejea Manchester United.

Lakini mreno huyo sasa ameiweka sokoni nyumba yake yenye vyumba vitano iliyopo kwenye eneo la Alderley Edge, Cheshire, kwa bei ya £3.75million.

Chanzo kimoja cha habari kilisema: “Mashabiki wa United  mara zote walikuwa wanajua hatua ya Ronaldo kutokuiuza nyumba yake iliyopo jijini Manchester ilikuwa ni kwa sababu alikuwa na mpango wa kurejea mjini labda kujiunga na United, lakini baada ya mwenyewe jana kuiweka sokoni nyumba hiyo - inayoonyesha matumaini ya Ronaldo kurudi Old Trafford yanazidi kufutika.